Wakati timu inapofanya vibaya ni rahisi kumtupia lawama kocha pasipo kuzingatia mazingira ambayo anakabiliana nayo
Msimu uliopita Miguel Gamondi aliiongoza Yanga kutetea taji la ligi kuu pia akaipeleka Yanga robo fainali ya ligi ya mabingwa baada ya kusubiri kwa miaka 25
Msimu huu akaanzia pale alipoishia msimu uliopita, timu yake imeanza vyema ligi ya mabingwa, ikafuzu hatua ya makundi na mapema pia ilitwaa Ngao ya Jamii
Licha mazingira magumu, akakiongoza kikosi chake kushinda mechi nane mfululizo za ligi kabla ya kupoteza dhidi ya Azam Fc na jana dhidi ya Tabora United
Lakini ni wazi Yanga kupoteza mechi hizi mbili kumechangiwa na mazingira ambayo yalikuwa nje ya uwezo wake kama kocha
Unafanyaje pale unapowakosa wachezaji wako muhimu kikosini? Sio kila siku timu itafanya vizuri inapowakosa nyota wake
Bahati mbaya kwake amekosa silaha zake zote katika safu ya ulinzi Bacca, Job, Yao na Boka. Jana alilazimika kumtumia Aucho eneo la beki wa kati baada ya Aziz Andambwile kuumia baada ya dakika 8 tu
Ikumbukwe pia kikosi chake kimetoka kucheza mechi ngumu dhidi ya Azam Fc ambayo walicheza pungufu kwa zaidi ya dakika 70 baada ya Bacca kutolewa nje kwa kadi nyekundu
Katika mikutano yake na wanahabari kuelekea mechi, Gamondi hakuacha kulalamikia ratiba. Ukweli ni kuwa wachezaji wengi wa Yanga wametumika sana pasipo kupata muda wa maandalizi ya mechi
Mechi zinapochezwa kila baada ya siku tatu maana yake ni kuwa hakuna muda wa kufanya mazoezi ya kitaalam kuimarisha 'fitness' ya wachezaji
Kwa sababu pengine mechi inayofuata unapaswa kusafiri kwenda kucheza ugenini hivyo unakuta ni siku moja au mbili tu za mazoezi ya kawaida kabla ya kucheza mechi nyingine
Lakini pia Yanga imeathirika kwa nyota wake wengi kuitwa timu za Taifa. Wachezaji hawapati muda wa kupumzika kwani baada ya kumaliza majukumu ya timu za Taifa, wanakutana na bandika bandua ya ratiba ya ligi kuu, baada ya mwezi wanatakiwa tena kwenda timu ya Taifa na utaratibu umekuwa hivyo katika kipindi cha miezi mitatu mfululizo
Gamondi amekumbana na nyakati ngumu, naamini atatafuta njia ya kukabiliana na changamoto hizi ili kuhakikisha anairejesha Yanga katika ubora