Taarifa ya Yanga kuhama uwanja wa Azam Complex, ilianza kama tetesi mitandaoni hatimaye jana ikathibitishwa rasmi Wananchi kuhamia uwanja wa KMC Complex
Ni maamuzi yaliyofikiwa baada ya Kamati ya Utendaji ya Yanga kujiridhisha uwanja wa Azam Complex sio salama tena kwa Yanga msimu huu
Uamuzi wa Yanga kuhama Azam Complex haukutokea tu bali uliokuwepo hata kabla Yanga kupoteza mechi mbili za ligi kuu dhidi ya Azam Fc na Tabora United
Ushirikiano mdogo kutoka kwa wamiliki wa uwanja na matukio tata yanayohusishwa na kuihujumu Yanga, ni miongoni mwa sababu zilizopelekea Yanga kufikia uamuzi huo
Mara kadhaa Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi aliweka wazi kutofurahia kucheza katika uwanja huo unaomilikiwa na Azam Fc ambayo ina malengo ya kutwaa ubingwa kama ilivyo Yanga
"Hapa sio uwanja wetu wa nyumbani, ni uwanja wa Azam Fc ambao tunalazimika kucheza kwa sasa," alisema Gamondi katika moja ya mahojiano yake
Yanga haitarajii kuhujumiwa KMC Complex kwa sababu uwanja huo ni mali ya Serikali kama ulivyo uwanja wa Benjamin Mkapa
Uwanja wa KMC Complex unamilikiwa na Manispaa ya Kinondoni, Yanga na klabu nyingine zinaruhusiwa kuutumia