Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe akiongozana na baadhi ya Wanachama na Mashabiki mapema leo walitinga uwanja wa KMC Complex kwa kile alichoeleza kufanya usafi na kuhakikisha uwanja uko tayari kwa ajili ya mechi za Yanga
Juzi Yanga ilitangaza kuhamia dimba la KMC Complex wakiukacha uwanja wa Azam Complex ambao wameutumia kama uwanja wao wa nyumbani tangu msimu uliopita
"Tumekuja hapa kukagua uwanja na kufurahia maamuzi ya viongozi wetu kuhamia hapa, naamini tutafanya vizuri katika uwanja huu"
"Tunawakaribisha rasmi Wanachama na Mashabiki wa Yanga katika uwanja huu kwani sasa mechi zote zilizobaki kwenye ligi ambazo tutacheza nyumbani pamoja na kombe la FA tutacheza katika uwanja huu"
"Niwaambie tu, hapa Prince Dube atafunga sana, maana hakuna mambo ya kupunguza mwanga...," alitamba Kamwe
Nae Jimmy Kindoki ambaye ni Afisa wa usajili wa Wanachama na Mashabiki amesema kitendo cha Yanga kuhamia KMC Complex kitatoa ahueni kwa mshabiki ambao walikuwa wakikabiliwa changamoto ya foleni kufika Chamazi
"Miundombinu hapa iko vizuri kuliko Chamazi. Kule ilikuwa kwa mechi inayochezwa saa 1 shabiki unalazimika kutoka nyumbani saa 5 kama unataka kuwahi sababu ya foleni"
"Lakini hapa panafikika kwa urahisi wakati wowote. Uwanja huu pia ni mkubwa kulinganisha na ule tuliokuwa. Idadi ya mashabiki wanaoingia hapa ni wengi kuliko Azam Complex. Eneo la kuchezea 'pitch' pia liko vizuri sana hapa"
"Hapa mechi zinachezwa mapema hakuna changamoto ya mwanga, kiufupi uwanja 'haukonyezi' kama kule tulipotoka," alisema Kindoki