Kocha Mkuu wa Yanga Princess Edna Lema amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba Queens ambao utapigwa kesho Jumatano katika uwanja wa KMC Complex
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari mapema leo kuelekea mchezo huo, Lema amesema licha ya kikosi chake kuanza ligi kwa kusuasua lakini wamejipanga kuhesabu ushindi wao wa kwanza msimu huu dhidi ya Simba Queens
Lema amesema anatambua wapinzani wao wameanza vyema msimu kwa kushinda mechi zote tatu, lakini wasitarajie mchezo mwepesi hapo kesho
"Sisi kama timu tumejiandaa vizuri. Simba ni timu bora tunaiheshimu. Hatujapata matokeo mazuri hivyo tunao wajibu wa kuhakikisha mchezo unaokuja tunashinda. Mechi yetu na Simba ni mechi mpya, ni mechi ngumu sana kuitabiri kwa kuangalia matokeo yaliyopita. Hatuna matokeo mazuri hivi karibuni lakini hii ni mechi mpya"
"Simba wameshinda mechi tatu lakini haimaanishi kuwa mchezo ujao kwao utakuwa rahisi. Tunajua watakuja kwa tahadhari vile vile. Rai yangu ni kwa mashabiki wajitokeze kwa wingi kuipa timu yetu hamasa ya kutosha. Hatupaswi kuwa na hofu kwa kutazama matokeo yetu ya awali"
"Tunapaswa kuonesha ubora wetu kama Yanga kwa kuhakikisha tunashinda mchezo huu Derby ili kutunza heshima yetu. Tunataka kuweka hadhi ya Derby hii kubwa ya Tanzania na watu wajue Derby sura sahihi ya Derby hii. Isiwe ni Derby ya upande mmoja. Kazi yetu kesho ni kuonesha kuwa tumeandaa timu nzuri yenye uwezo wa kushindana na timu yoyote ile," alisema Lema