Katika misimu miwili iliyopita, Yanga haikuwa na mwanzo mzuri kwenye michuano ya ligi ya mabingwa na kombe la Shirikisho ikipoteza mechi za ufunguzi
Msimu uliopita mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ligi ya mabingwa, Yanga ilianzia ugenini dhidi ya CR Belouizdad Wananchi wakikubali kipigo cha mabao 3-0
Haukuwa mwanzo mzuri kwa Yanga ambayo ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly kabla ya kulazimishwa sare nyingine dhidi ya Medeama na kisha kushinda mechi mbili zilizofuata dhidi ya Medeama na CR Belouizdad na kujihakikishia kutinga robo fainali
Msimu wa2022/23 pia mechi ya kwanza makundi ya kombe la Shirikisho Yanga ilianza kwa kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Monastir ya Tunisia kabla ya kushinda mechi iliyofuata dhidi ya TP Mazembe, ikalazimishwa sare dhidi ya Stade De Malien na kisha kushinda mechi zilizofuata dhidi ya Stade Malien, Monastir na TP Mazembe na kujihakikishia tiketi ya robo fainali kwa kuongoza kundi
Ni katika msimu ambao Yanga ilicheza fainali ya kombe la Shirikisho na kukosa kombe kwa mujibu wa kanuni baada ya sare ya mabao 2-2 katika mechi mbili za fainali dhidi ya USM Alger
Safari hii Yanga inaanzia nyumbani hatua ya makundi ligi ya mabingwa dhidi ya Al Hilal mchezo utakaopigwa Novemba 26 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Takwimu hizi za misimu miwili iliyopita zimempa mwanga Kocha Miguel Gamondi kuelekea mchezo dhidi ya Al Hilal
Gamondi alikiongoza kikosi cha Yanga msimu uliopita kule Algeria wakati kikipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad
Wakati huu Yanga inahitaji kuanza vyema nyumbani kwa kuibuka na ushindi ili kumaliza 'jinamizi' la kupoteza mechi ya kwanza katika michuano hiyo
Lakini pia kwa Gamondi huu ni mtihani ambao anahitaji kufaulu kwani kikosi chake kimetoka kupoteza mechi mbili za ligi kuu, hakuna nafasi ya kupoteza mechi ya tatu mfululizo