Baada ya kufunga bao lililoipatia Yanga alama moja muhimu kule Lubumbashi katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya TP Mazembe uliopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita, mshambuliaji Prince Dube leo ana nafasi ya kuendeleza makali yake pale Yanga itakapoikabili Mashujaa Fc katika mchezo wa ligi kuu utakaopigwa uwanja wa KMC Complex
Wanasema kwa mshambuliaji mzuri anayepita katika kipindi kirefu cha ukame wa mabao, huhitaji kufunga bao moja tu ili kurejea katika uwezo wake wa kuzifumania nyavu
Dube alianza vyema msimu akiifungia Yanga katika mechi za pre-season, ngao ya Jamii na hatua za awali ligi ya mabingwa
Katika mechi za awali alipotua Yanga, Dube alifunga takribani mabao matano na kutoa pasi mbili za mabao
Lakini baada ya ligi kuanza, mambo hayakuwa mazuri upande wake, katika mechi 11 pamoja na kwamba hakuanza katika baadhi ya mechi, hakufanikiwa kuzifumania nyavu
Huyu ni mshambuliaji ambaye mpaka anaondoka Azam Fc katikati ya msimu uliopita, alikuwa amepachika mabao 8
Ameanza kufunga tena katika mechi ya ligi ya mabingwa na sasa anachohitaji ni kufunga bao lake la kwanza kwenye ligi msimu huu
Bila shaka kocha Sead Ramovic leo atampa nafasi Dube kwa kuzingatia alifanya nyema dakika chache alizomtumia katika mechi dhidi ya TP Mazembe