Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema wachezaji wote ambao walisafiri na timu Mauritania katika mchezo dhidi ya Al Hilal, wamerejea wakiwa imara kuelekea mchezo wa Jumamosi dhidi ya MC Alger kuhitimisha hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa
Kamwe amesema hali za wachezaji waliobaki jijini Dar es salaam kutokana na majeraha afya zao zimeimarika, ni mchezaji mmoja tu ambaye atakosekana
"Yao KouassiΒ amefanyiwa upasuaji wa goti na enka, anaweza kuwa nje ya uwanja kwa wiki nne hadi sita. Kouasi hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachoikabili MC Alger siku ya Jumamosi"
"Maxi Nzengeli amerejea kikosini na anashiriki mazoezi na wachezaji wengine. Kama kocha Ramovic atajiridhisha na utimamu wake, basi atatumika katika mchezo huo," alisema Kamwe
Akizungumzia sintofahamu kuhusu ujio wa MC Alger, Kamwe amesema hawafahamu timu hiyo itawasili lini
"MC Alger walitoa taarifa ya kuwasili alfajiri ya kuamkia leo lakini hawakufika. Klabu ya Yanga imetimiza wajibu wake ikiwa ni pamoja na kutuma wawakilishi kuipokea timu hiyo JNIA"
"Yanga imewasiliana na ubalozi wa Algeria nchini ambapo wametujuza wanazo taarifa za ujio wa MC Alger ikiwa ni pamoja na muda ambao watawasili," aliongeza Kamwe
Kamwe amewapongeza mashabiki na wanachama wa Yanga kwa muitikio wao mkubwa katika ununuzi wa tiketi
Mpaka sasa tiketi za VIP A zimemalizika huku VIP B zikielekea ukiongoni. Kamwe amewataka wananchi kuendelea kununua tiketi zao mapema
"Yanga inahitaji kujaza uwanja wa Benjamin Mkapa. Kama kuna ujumbe tutautuma kwa wachezaji wetu, ni kujaza uwanja wa Benjamin Mkapa"
"Kama kuna ujumbe tunataka kutuma Afrika basi ni kujaza uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumamosi"
"Miezi michache nyuma tulikuwa tukizungumza hatuna pointi hata moja baada ya mechi mbili. Tukapata pointi moja baada ya mechi ya tatu"
"Lakini sasa tunakwenda kucheza mechi ya kuamua hatma ya kufuzu robo fainali. Tunahitaji ushindi wa aina yoyote ili tufuzu"