Mapema leo Yanga ilizindua Kampeni ya Hamasa na tamasha la Shabiki Cup Mbagala Zakiem ikiwa ni shamrashamra kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya MC Alger utakaopigwa Jumamosi, Januari 18 uwanja wa Benjamin Mkapa
Kupitia uzinduzi huo mashabiki wa Yanga walishuhudia na kushiriki matukio mbalimbali ya burudani, kukata tiketi huku Shabiki Cup ikitoa fursa kwa vijana kuonesha vipaji vyao
Akizungumza katika Tamasha hilo, Abbas Tarimba Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Yanga ambaye pia Mkurugenzi wa SportPesa Tanzania waliodhamini Shabiki Cup, amewapongeza viongozi wa Yanga kwa kujitoa na kushiriki Tamasha hilo huku akiwataka mashabiki kununua tiketi ili kujaza uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo dhidi ya MC Alger
“Niwapongeze viongozi wa klabu ya Yanga kwa kujitoa kushiriki katika tamasha la uvumbuzi wa vipaji la Shabiki Cup. Tamasha hili linatoa fursa kwa vijana kuonesha vipaji vyao pengine huenda wakachukulia na klabu ya Yanga au klabu nyingine”
“Nawaomba sana wanachama na wapenzi wa Yanga kujitokeza kwa wingi siku ya Jumamosi kwenye mechi ya Yanga na MC Alger. Ni matumaini yangu mtaujaza uwanja, kwa wale ambao hawatapata nafasi ya kwenda uwanjani basi watumie muda wao mwingi kuiombea Yanga ifanye vizuri. Yanga ikifanikiwa kutinga robo fainali ni faida kubwa kwa taswira ya soka la Tanzania,” alisema Tarimba