Yanga imeendeleza vipigo ligi kuu ya NBC leo ikiichapa Kagera Sugar mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa KMC Complex
Yanga iliuanza mchezo huo kwa kasi na alikuwa ni Clement Mzize aliyewatanguliza Wananchi kwa bao safi ya dakika ya 32 akimalizia pasi murua ya Stephane Aziz Ki baada ya Yanga kuwanyang'anya mpira Kagera Sugar katika eneo lao la hatari
Aziz Ki alikuwa na nafasi ya kuongeza bao la pili dakika chache baadae kupitia mkwaju wa penati
Hata hivyo kwa mara nyingine Aziz Ki amekumbushwa kufanyia kazi umahiri wake katika kupiga penati leo akikosa nyingine
Ulikuwa mchezo wa upande mmoja kwa muda mwingi Yanga ikiendelea kutawala katika kipindi cha pili
Mudathir Yahya akaongeza la pili dakika ya 60 kabla ya Pacome kuongeza la tatu kupitia mkwaju wa penati katika dakika ya 78
Bao la nne liliwekwa kimiani na Kennedy Musonda akimalizia krosi ya Maxi ambaye kuingia kwake katika kipindi cha pili pamoja na Pacome, Chama na Musonda kuliongeza kasi ya mashambulizi
Ni ushindi ambao umeipeleka Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha alama 42 mbele ya watani zao Simba wenye alama 40 wakitarajiwa kushuka dimba kesho dhidi ya Tabora United