Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Singida Black Stars ambao utapigwa uwanja wa KMC Complex hapo kesho
Akizungumza katika Mkutano na wanahabari mapema leo, Hamdi alisema licha ya kuwa na timu bora, watacheza mchezo huo kwa umakini mkubwa na kuwaheshimu wapinzani
Hamdi amesema anafahamu Singida BS ni timu nzuri yenye wachezaji bora lakini wamejiandaa vyema kukabiliana na mchezo huo mgumu lengo likiwa kuibuka na ushindi
"Tumejiandaa kama ambavyo tumejiandaa mchezo uliopita. Tunafahamu ni mchezo mgumu na muhimu hivyo tumeongeza umakini mkubwa. Mchezo uliopita tulikuwa mchezo mzuri sana dhidi ya KMC FC, mpango wetu ni kucheza vile vile isipokuwa tunapaswa kuwa makini zaidi"
"Tunafahamu Singida ni timu nzuri sana ina wachezaji wenye ubora wa hali ya juu, lakini ni matumaini kuwa tutakuwa na mchezo mzuri uwanjani. Nitaangalia vitu gani napaswa kubadilisha kwenye kikosi changu"
"Utakumbuka hatukucheza vizuri dhidi ya JKT lakini Singida wao walishinda, huo ndio mpira wa miguu. Hata hivyo mimi sio muumini mkubwa wa takwimu zilizopita. Unaweza kuwa na mchezo mzuri leo kesho ukawa na mchezo mbaya"
"Wanaonifahamu wanajua namna gani nina kuwa na uchu wa kupata ushindi, lakini hilo haliondoi ukweli kwamba tunapaswa kuwaheshimu wapinzani"
"Nikisema nawaheshimu wapinzani haimaanishi nina hofu, namaanisha mpira ni mchezo wa ushindani na kila mtu anatumia mbinu mbalimbali kujaribu kushinda hivyo lazima niende kwa tahadhari na umakini hata kama nahitaji kupata alama tatu," alisema Hamdi
Katika hatua nyingine, Hamdi amesema Jonathan Ikangalombo bado hayuko tayari kutumika katika mchezo huo licha ya kuwa tayari ameanza mazoezi na wenzake
"Jonathan ni mchezaji wa Yanga na kila mtu anajua ubora alio nao, nilisema siku tatu zilizopita kwa sasa hayupo tayari na mimi malengo yangu nimeyaweka kwa wachezaji ambao wapo tayari kutumika kwa kipindi hiki," alisema