Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema maandalizi kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba utakaopigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa yanaendelea vizuri huku wachezaji wakiwa na ari kubwa kuelekea mchezo huo
Baada ya kusambaa tetesi za kufungiwa, jana jioni Kamwe akaibukia Avic Town kushuhudia mazoezi akiungana na viongozi wengine waandamizi wa Yanga wakiongozwa na Rais wa klabu Injinia Hersi Said pamoja na Mdhamini/Mfadhili wa Yanga, GSM
Kamwe amesema Yanga inakwenda katika mchezo huo ikiwa kwenye nyakati bora kwani kila mchezaji yuko tayari na 'anautaka mchezo'
"Timu iko tayari, kila mchezaji ana ari kubwa kuelekea mchezo huu muhimu sana kwetu. Mimi sio mtu wa kuzungumza tu kufurahisha watu lakini kwa maandalizi niliyoyaona hapa, nikwambie tu watakuwa na kazi Jumamosi"
"Mara nyingi mazingira yanapokuwa hivi hapa Avic Town basi ujue Wananchi wanakwenda kufurahi"
"Wachezaji wetu wako tayari, sasa ni jukumu letu mashabiki kuhakikisha tunakata tiketi kwa wingi ili kuwaongezea hamasa zaidi ili wahakikishe tunashinda mchezo," alisema Kamwe
Kauli ya GSM siku zote ni Yanga Bingwa, kuhakikisha kauli hiyo inatimia kwa msimu wa nne mfululizo, GSM jana aliweka kambi Avic Town kushuhudia kila hatua ya maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya Simba
Mara nyingi GSM anapoonekana Avic Town, nyuso za wachezaji hujaa furaha kwani wanafahamu ushindi unakwenda kuzifanya akaunti zao 'zinone bonasi'