Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo katika raundi ya 23 mchezo mmoja ukitarajiwa kupigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa. Ni Kariakoo Derby itakayozikutanisha timu zenye upinzani wa jadi, Yanga na Simba
Kumekuwa na mambo mengi nje ya uwanja wiki yote hii kuelekea mchezo huo. Usiku wa kuamkia leo klabu ya Simba ikatoa taarifa kuwa haitashiriki mchezo huo ikidai jana ilinyimwa haki ya kufanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Benjamin Mkapa kama kanuni zinavyoelekeza
Hata hivyo wadadisi wa mambo wanaamini hizo ni 'mind games' ambazo Simba wanafanya, mchezo utapigwa saa 1:15 usiku kama ulivyopangwa
Kwa mujibu wa kanuni, kama Simba haitatokea uwanjani, Yanga itapewa alama tatu na mabao matatu na pengine Simba watakumbana na adhabu kubwa zaidi
Kushindwa kufanya mazoezi ya mwisho katika uwanja husika sio miongoni mwa sababu ambazo zinaweza kuhalalisha timu kugomea mchezo
Kama itabainika kuna makosa yalifanyika yaliyopelekea Simba kukosa nafasi ya kufanya mazoezi ya mwisho, wahusika wataadhibiwa kwa kuzingatia kanuni lakini pia timu iliyogoma kwenda kucheza mechi itaadhibiwa kwa kuzingatia kanuni pia!
Uwanja wa Benjamin Mkapa unamilikiwa na Serikali na sio klabu ya Yanga, iko wazi Meneja wa uwanja ndiye aliyewazuia Simba kufanya mazoezi kwa kuwa hakuwa na taarifa za ujio wao
Hata Yanga ambayo ni timu mwenyeji haikufanya mazoezi katika uwanja huo na imekuwa hivyo katika dabi zote, halikuwahi kutokea tukio la aina hii
Mechi ya mwisho kuzikutanisha timu hizo ambayo ilipigwa Oktoba 19 Simba akiwa mwenyeji, Yanga haikupewa nafasi ya kufanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Benjamin Mkapa na haikutangaza kugomea mechi kama walivyofanya watani zao
Ni wazi mechi itapigwa katika muda uliopangwa, wale ambao hawana tiketi wanunue tiketi zao mapema kwani hii mechi ipo..!