Kauli aliyoitoa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia juu ya madai ya Yanga kukosa imani na baadhi ya viongozi wa Bodi ya Ligi na kuwataka wajiuzulu, imewaacha na sintofahamu Wanachama na Mashabiki wa Yanga juu ya hatma ya madai yao
Akihojiwa katika kipind cha Game Plan EFM radio, Karia hakuunga mkono matakwa ya viongozi wa Bodi wajiuzulu akidai hakuna kiongozi asiyefanya makosa
Karia aliwataka wadau wa michezo waache taratibu zifuatwe kwa kuzingatia kanuni na sio kusema tu Bodi ijiuzulu
"Taratibu zitafuatwa na tuziache zifuatwe, lakini huwezi kusema bodi ijiuzulu. Hata wanaosema bodi ijiuzulu wawaambie na Viongozi wao wenyewe wako sawa sawa? Hawastahili kujiuzulu?," alihoji Karia
Yanga iliandika barua TFF ambapo kati ya madai yake ni pamoja na kuwataka Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Steven Mnguto na Mtendaji Mkuu Almas Kasongo wajiuzulu kwa kushindwa kusimamia kanuni baada ya kuahirisha mchezo dhidi ya Simba pasipo kuwa na sababu za msingi
Yanga pia iliomba kupewa alama tatu za mchezo huo baada ya Simba kugomea mchezo huo kwa kile walichodai walinyimwa nafasi ya kufanya maandalizi yao ya mwisho katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Lakini pia Wananchi waliweka msimamo hawatakuwa tayari kucheza mchezo huo katika tarehe nyingine yoyote ambayo itapangwa kwa kuwa wanaamini hakukuwa na sababu za msingi kuahirisha mchezo na kuwa shinikizo la kuahirishwa kwake lilitokana na madai ya Simba ambayo hayana msingi wa kikanuni kusababisha mechi kuahirishwa
Yanga ilitoa siku tatu kupatiwa majibu ya madai yao, ukimwa unaanisha hatua inayofuata ni kulifikisha shauri hilo katika mamlaka za juu (CAS)
Tangu mchezo huo ulipoahirisha March 08, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na Bodi ya Ligi licha ya kuwa walidai watatoa taarifa baada ya kukamilisha uchunguzi wa madai ya Simba