Baada ya kurejea kutoka Singida ambako juzi Jumatatu walishiriki tukio la uzinduzi wa uwanja wa Airtel unaomilikiwa na Singida Black Stas, kikosi cha Yanga kinarejea mazoezini kwa ajili ya maandalizi ya mechi zinazofuata
Jumamosi March 29 Yanga itashuka uwanja wa KMC Complex kumenyana na Songea United katika mchezo wa hatua ya 16 bora kombe la Shirikisho la CRDB kisha kuelekea mkoani Tabora kuikabili Tabora United kwenye mchezo wa ligi kuu utakaopigwa April 1
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema kwa sasa wamezielekeza nguvu zao kwenye mchezo dhidi ya Songea United, wakihitaji kushinda ili kutinga robo fainali ya CRDB Cup
"Mchezo wetu dhidi ya Songea United wanachama na mashabiki wetu wasitarajie kuona mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha kwanza kwani wachezaji ambao watatumika ni wale ambao wameonyesha jitihada kwenye uwanja wa mazoezi na kumshawishi Mwalimu kwamba wanatosha kwenye mipango ya mechi hiyo"
"Kwa sasa hatuna muda wa kucheka na yeyote au kudharau timu yoyote, malengo yetu yanatuongoza kuongeza umakini na kuwa na utayari wa kupambana dhidi ya mpinzani yeyote anayekuja mbele"
"Niwaambie Songea United, wanakuja kucheza na Yanga yenye malengo ya kutetea taji la Shirikisho la CRDB kwa msimu wa nne mfululizo"
Kamwe amesema wachezaji wote katika kikosi wanaendelea na program za mazoezi ya timu isipokuwa Yao Kouassi ambaye bado anafanya program maalum za mazoezi binafsi kurejesha utimamu wa mwili kabla ya kuanza mazoezi na wachezaji wengine