Nahodha msaidizi wa Yanga, Dickson Job, amesema kikosi cha Yanga kimejiandaa kikamilifu kwa pambano la Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Azam FC litakalochezwa Alhamisi, Aprili 10, kwenye dimba la Azam Complex kuanzia saa 1 usiku
Akizungumza na wanahabari kuelekea mchezo huo wa mzunguko wa pili wa ligi, Job alisema morali ya wachezaji iko juu na kila mmoja ana hamasa kubwa kuhakikisha wanatoka na ushindi muhimu katika safari ya kutetea taji lao la nne mfululizo
"Wachezaji wote wako fiti, tumejiandaa vizuri na tunajua umuhimu wa mchezo huu. Lengo letu ni moja tu—kushinda," alisema Job kwa kujiamini
Yanga, ambayo inaongoza ligi kwa alama 64, inasaka taji la nne mfululizo la Ligi Kuu ya NBC. Ikiwa zimesalia mechi tano kabla ya msimu kumalizika, ushindi dhidi ya Azam FC unaweza kuwa hatua kubwa kuelekea kutimiza azma hiyo
Hata hivyo, Job alikiri kuwa hawatasahau yaliyowakuta katika duru ya kwanza walipofungwa bao 1-0 na Azam FC
"Tunatambua tulifanya makosa kwenye mchezo wa duru ya kwanza. Azam walitufunga kwa kutumia makosa yetu, lakini safari hii tumejipanga kuhakikisha hatuyarudii tena," alisisitiza Job
Katika msimamo wa ligi, wapinzani wakuu wa Yanga—Simba SC—wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama 57, lakini wakiwa na mechi mbili mkononi
Azam FC nao bado wapo kwenye mbio za nafasi ya tatu, wakiwa na pointi 51 na matumaini ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao
Job alisema kuwa licha ya ushindani kutoka kwa Azam FC na Simba SC, Yanga haitazami nyuma wala kushikwa na presha, bali wanajikita kwenye maandalizi na kuhakikisha wanadhibiti hatma yao wenyewe
"Hatuangalii tulipo, tunaangalia tunakokwenda. Tunajua kila mechi ni fainali kwetu, na tunaamini uwezo wa kikosi chetu unaweza kutufikisha pale tunapotaka kufika"
Mchezo wa Alhamisi unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua, ukiwaleta pamoja wapinzani wa aina yake katika soka la Tanzania katika pambano lenye uzito wa pointi tatu na fahari ya mji wa Dar es Salaam