Azam FC na Yanga wanatarajiwa kuvaana leo Alhamisi, Aprili 10, 2025, saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex katika mchezo muhimu wa Ligi Kuu ya NBC
Yanga, mabingwa watetezi, wanaongoza msimamo wa ligi kwa pointi 64 na wanahitaji kushinda ili kuendeleza mwenendo wao mzuri na kusogea karibu zaidi na kutetea taji lao
Azam FC wapo nafasi ya tatu kwa pointi 51, vita yao kubwa ni kumaliza katika nafasi nne za juu ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Kimataifa msimu ujao kwani nafasi yao kutwaa ubingwa ni finyu
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Novemba 2, 2024, Azam FC waliibuka na ushindi wa bao 1-0. Hata hivyo, mapema katika fainali Ngao ya Jamii kuelekea msimu huu Yanga ilitwaa Ngao mbele ya Azam Fc kwa kuichapa mabao 4-1
Mechi kati ya timu hizi kwa kawaida huwa na ushindani mkubwa na inatarajiwa kuvutia mashabiki wengi kutokana na historia yao
Wachezaji wa Kuangaliwa Kwa upande wa Yanga, washambuliaji Prince Dube na Clement Mzize wamekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu, kila mmoja akiwa na mabao 11 – wakisalia nyuma kwa bao moja tu dhidi ya kinara wa mabao wa ligi
Uwezo wao wa kufumania nyavu utakuwa muhimu sana kwa kikosi cha Yanga leo. Kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki, ambaye alikosa mechi mbili zilizopita kutokana na majeraha, huenda akarudi kwenye kikosi na kuongeza ubunifu katika safu ya ushambuliaji
Pacome Zouzou ameiongoza Yanga kushinda mechi tatu mfululizo ambayo yeye aliibuka nyota wa mchezo. Ni wazi leo Wananchi watahitaji 'uprofesa' wake ufanya kazi pale Chamazi
Mabeki Ibrahim Bacca na Chadrack Boka ambao walipumzishwa katika mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union nao wanatarajiwa kurejea kikosini
Kwa Azam FC, kiungo Feisal Salum "Fei Toto" amekuwa na msimu mzuri, akichangia kwa kiwango kikubwa katika mashambulizi ya timu yake. Yeye na Gibril Sillah ndio wachezaji ambao Yanga itapaswa kuwachunga ili wasisababishe madhara.
Sillah amekuwa na 'bahati' ya kuifunga Yanga mara kwa mara akifunga bao pekee la Azam Fc mara ya mwisho timu hizo zilipokutana Azam Complex
Kwa kuwa zimesalia mechi sita tu kumaliza msimu, mchezo huu una umuhimu mkubwa. Ushindi kwa Yanga utawaimarisha kileleni na kuwa katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa