Jana klabu ya Yanga iliendeleza ubabe wake katika michuano ya Kombe la CRDB baada ya kuicharaza Stand United kwa mabao 8-1 katika mchezo wa robo fainali uliochezwa katika uwanja wa KMC Complex
Mabingwa watetezi hao walionyesha soka safi la kuvutia huku viungo washambuliaji Clatous Chama na Stephane Aziz Ki wakiongoza mashambulizi yaliyosambaratisha kabisa safu ya ulinzi ya Stand United
Aziz Ki aling’ara vilivyo kwa kufunga mabao manne na kutoa pasi mbili za mabao, kiwango kilichomfanya aondoke na tuzo ya nyota wa mchezo
Aidha Chama nae akadhihirisha umuhimu wake katika kikosi cha kocha Miloud Hamdi akifunga mabao mawili na kutoa asisti mbili kwa Aziz Ki
Ushirikiano wao wa hali ya juu pamoja na wachezaji wengine, ulibeba timu na kuibua shangwe kwa mashabiki wa Yanga waliokuwa na matumaini makubwa ya ushindi katika mchezo huo
Bao hizo nane zimeiweka Stand United kwenye rekodi ya kuwa timu iliyofungwa mabao mengi zaidi katika michuano hiyo kwa msimu huu, jambo linalodhihirisha ukubwa wa pengo la kiufundi kati ya timu hizo mbili
Kwa matokeo haya, Yanga SC imesonga mbele hadi hatua ya nusu fainali ambapo sasa itavaana na maafande wa JKT Tanzania katika mchezo unaotarajiwa kuwa wa kuvutia pia
Yanga, ambayo ni bingwa mtetezi wa kombe hilo kwa misimu mitatu mfululizo, inaonekana kuwa kwenye njia sahihi ya kutetea tena taji lake