Msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2024/25 una kila sababu ya kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu za soka la Tanzania lakini kwa sababu ambazo mashabiki wengi wa mpira hawangependa kuona.
Badala ya kusimulia ushindani wa kuvutia, mabao ya kiufundi, au vipaji vinavyoibukia, msimu huu umetawaliwa na malalamiko ya maamuzi tata, ukosefu wa usawa, na matukio ya vurugu yanayotia doa taswira ya mpira wa miguu nchini.
Yanga na Safari ya Ubingwa Lakini Kwa Bei Gani?
Iwapo Yanga SC watatwaa ubingwa wa msimu huu, basi itakuwa ni moja ya misimu ambayo mashabiki wake wana kila sababu ya kusherehekea kwa nguvu. Hii ni kutokana na changamoto na mazingira tata ambayo timu hiyo imekabiliana nayo.
Licha ya kuwa na kikosi bora na kuonyesha kiwango kizuri uwanjani, mara nyingi mijadala baada ya mechi zao imejikita kwenye soka safi waliocheza tofauti kabisa na kile kinachoonekana kwa wapinzani wao wakuu, Simba SC.
Kwa upande wa Simba, mjadala mara nyingi huwa hauhusiani na soka uwanjani bali na waamuzi. Kumekuwa na matukio mengi ya ‘makosa ya kibinadamu’ yanayojirudia kwenye mechi zao mengi yakiwa yamejaa utata, huku faida kubwa ikionekana kuelekezwa upande mmoja. Wadau wa soka wamekuwa wakilalamika waziwazi, lakini mamlaka husika zimekaa kimya.
Mashabiki na Vurugu: Mpira Unapopoteza Uungwana
Msimu huu haujashuhudia tu changamoto za kiutawala na upendeleo, bali pia ongezeko la vitendo vya vurugu uwanjani. Jumapili iliyopita, mashabiki wa Yanga waliokwenda kushuhudia fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba na RS Berkane walijikuta wakikumbwa na madhila makubwa wengine walipigwa, wengine kuondolewa kwa nguvu, na hata kuchaniwa jezi zao na mashabiki wa Simba. Matukio haya yamethibitishwa kwa ushahidi wa picha na video.
Hali haikuishia hapo kwenye uwanja wa KMC Complex, mashabiki wa Simba walinaswa wakiwarushia wachezaji wa Singida Black Stars makopo ya maji, tukio lililotokea mbele ya waamuzi bila hatua yoyote kuchukuliwa. Hili linaibua maswali makubwa kuhusu usalama wa wachezaji, heshima ya sheria 17 za FIFA, na uaminifu wa mfumo wa ligi yetu.
Sakata la Mechi ya Yanga na Simba: Kanuni Zapuuzwa?
Kwa mujibu wa ratiba, Yanga walitakiwa kucheza dhidi ya Simba Juni 15, lakini mechi hiyo imeingia katika utata mkubwa. Simba waligoma kucheza mechi ya awali kwa madai ya kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa mechi madai ambayo hayana msingi wa kikanuni.Kinachoshangaza zaidi, mamlaka zimepanga tarehe mpya bila kutoa sababu rasmi ya kuahirishwa kwa awali.
Kwa kulijibu hili, Yanga wamesimamia kanuni na kusisitiza kuwa hawatacheza mechi hiyo hadi haki na utaratibu utakapozingatiwa. Kwao, kucheza mechi hiyo katika mazingira hayo ni sawa na kuhalalisha matendo wanayoyapinga. Zaidi ya hayo, wameonya kuwa mechi hiyo ikiendelea bila kushughulikiwa kwa ukiukwaji uliofanyika, inaweza kuwa na madhara makubwa hata kusababisha maafa.
Ni Wapi Tunapopeleka Mpira wa Miguu?
Msimu huu unaacha maswali mengi kuliko majibu. Je, haki bado inazingatiwa kwenye soka letu? Je, mamlaka zinatoa ulinzi sawa kwa klabu zote? Je, mashabiki wataendelea kuvumilia vurugu na upendeleo kana kwamba ni sehemu ya mchezo?
Ikiwa tunataka Ligi Kuu NBC kuwa na hadhi ya kimataifa, basi lazima tuanze na msingi wa haki, usawa na heshima kwa kanuni. La sivyo, msimu huu wa 2024/25 utabaki kuwa kumbukumbu chungu kwenye historia ya soka la Tanzania kumbukumbu ya kile ambacho hakikutakiwa kutokea.