Katika kipindi cha misimu mitatu, Yanga SC imeweka rekodi ya aina yake katika soka la Tanzania kwa kutwaa karibu mataji yote ya ndani yaani Ligi Kuu Tanzania Bara(x3), Kombe la FA(x3), Ngao ya Jamii(x3) β na hata mataji ya kimataifa kama Toyota Cup nchini Afrika Kusini.
Lakini pamoja na mafanikio hayo ya kuvutia, swali linaibuka: Je, mafanikio haya ni tatizo?
Shamrashamra zilizotikisa Afrika
Yanga haikushinda tu, bali imetambulisha kawaida mpya ya kusherehekea ubingwa. Parade ya mabasi ya wazi (open-top buses), maelfu ya mashabiki mitaani, muziki, fasheni, na usanii yote haya yameifanya Yanga kuwa klabu ya kwanza Tanzania kufanya maadhimisho ya ubingwa kwa kiwango kinachofanana na vilabu vikubwa duniani
Picha na video kutoka kwenye shamrashamra za ubingwa wa msimu uliopita zilisambaa mtandaoni na kushangaza ulimwengu, si tu kwa idadi ya mashabiki, bali kwa ubunifu na mapenzi ya kweli kwa klabu.

Yanga haijafikia mafanikio haya kwa bahati nasibu. Chini ya usimamizi wa wadhamini kama GSM, klabu imepata uwekezaji mkubwa katika usajili, benchi la ufundi, miundombinu, na hata teknolojia ya kisasa katika maandalizi ya timu. Huu ni mpango wa muda mrefu wa kuifanya Yanga kuwa klabu ya kiwango cha kimataifa.
Kikosi cha Yanga kimekuwa na muunganiko wa vipaji vya ndani na nje ya nchi, huku wachezaji wakicheza soka la kuvutia, la kisasa, na lenye matokeo. Haijawahi kuwa suala la 'kubebwa', ushindi unapatikana kwa jasho, mbinu, na nidhamu.
Changamoto hazijaikosesha mwelekeo
Licha ya changamoto nyingi msimu huu, vikiwemo vikwazo vya ratiba, sintofahamu kuhusu baadhi ya mechi, na hata propaganda za kushusha morali, Yanga imesimama imara. Iko kileleni mwa msimamo wa ligi, tayari ipo fainali ya Kombe la CRDB, na imeshashinda Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano.
Hili linaonesha kuwa mafanikio haya hayakuja tu, ni matokeo ya mfumo, mikakati, na umoja ndani ya klabu.
Kwa sasa, Yanga inajivunia mataji 30 ya Ligi Kuu Tanzania Bara, rekodi ambayo inaipa hadhi ya kuitwa βMabingwa wa Kihistoria.β Na kwa jinsi mambo yanavyokwenda, klabu inaelekea kuongeza mataji mengine zaidi.
Mafanikio ya Yanga hayapaswi kuonekana kama tatizo, bali kama kigezo cha kujifunza kwa vilabu vingine. Badala ya kutumia njia za mkato, kulaumu, kubeza au kuanzisha propaganda, huu ni wakati wa kusoma ni nini kimeifanya Yanga kuwa na mafanikio haya makubwa, na namna ya kuyafikia kwa njia halali.
Kwa sasa, Yanga SC ni mfano halisi wa kilabu inayojengwa juu ya misingi imara ya kitaaluma, uzalendo, na ndoto kubwa