Katika hotuba yake ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26, iliyosomwa bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dk. Mwigulu Nchemba ametumia jukwaa hilo kutoa pongezi za dhati kwa mfadhili wa klabu ya Yanga, Ghalib Said Mohammed maarufu kama GSM, kutokana na mchango wake mkubwa katika mafanikio ya klabu hiyo kongwe nchini.
Dk. Nchemba alieleza kuwa mafanikio ya Yanga SC katika miaka ya hivi karibuni hayawezi kutenganishwa na uwepo wa GSM ambaye amewekeza kwa hali na mali kuhakikisha klabu hiyo inarejea katika ubora wake wa kihistoria.
“Nitumie fursa hii kumpongeza ndugu yangu Ghalib Said Mohammed 'GSM', ameleta chachu kubwa kwenye mafanikio ya Yanga,” alisema Dk. Nchemba mbele ya Bunge.
Waziri huyo pia alienda mbali zaidi kwa kuishauri klabu ya Yanga kuandaa mpango wa kumuenzi GSM kwa namna ya kipekee, ikiwa ni pamoja na kujenga sanamu lake katika uwanja mpya ambao klabu hiyo inapanga kuujenga eneo la Jangwani, yalipo makao makuu yao.
“Niwashauri Wanayanga wanapoandaa ramani ya ujenzi wa uwanja mpya, wasisahau kuweka sanamu kubwa la GSM,” aliongeza.

Katika kuonyesha mshikamano wa michezo kama kichocheo cha maendeleo na mshikamano wa kitaifa, Dk. Nchemba pia aliwataka viongozi wa vilabu vingine kujifunza kutoka kwa mafanikio ya Yanga na Simba SC kwa namna walivyoweza kujiendesha na kushindana kimataifa.
“Mafanikio wanayojivunia Simba sio mapya kwa Yanga kwani walifika hatua ya fainali mwaka juzi na walitolewa tu kwa uwiano wa goli la ugenini, hawakushindwa,” alisema kwa msisitizo, akionyesha jinsi soka linavyoweza kuleta heshima kwa taifa.
Tangu GSM alipoingia kuwekeza Yanga, klabu hiyo imeshinda zaidi ya mataji 10 yakiwemo mataji ya ligi kuu (x3), FA (x3), Ngao ya Jamii (x3) bila ya kusahau taji ligi ya Muungano waliloshinda msimu huu
Aidha GSM pia alifanikisha mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu 'Transformation' akigharamia mchakato mzima