Mikiki mikiki ya ligi kuu ya NBC inaendelea leo ambapo mechi nane za raundi ya 30 zitapigwa katika viwanja mbalimbali
Mabingwa watetezi Yanga watakuwa visiwani Zanzibar kukamilisha mzunguuko wa 30 kwa mchezo dhidi ya Dodoma Jiji utakaopigwa uwanja wa New Amaan Complex
Hii ni mechi muhimu kwa Yanga kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo
Kimahesabu Yanga inahitaja angalau alama nne katika mechi mbili zilizobaki ili kutwaa ubingwa
Lakini pia Wananchi wanaweza kubeba ubingwa leo kama watashinda ikiwa watani zao Simba watakosa ushindi katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar ingawa uwezekano huo ni mdogo kwa kuwa Kagera Sugar tayari wameshuka daraja hivyo mechi hiyo kwao ni ya kukamilisha ratiba tu
Katika Mkutano na wanahabari jana, Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi alisema ni lazima watumie vyema dakika 90 za mchezo wa leo kwa kuibuka na ushindi
"Mpaka sasa sisi hatufikirii ubingwa lakini kama tutashinda mchezo dhidi ya Dodoma Jiji basi tutaanza kufikiria kuwa mabingwa kwa sababu tutasalia na mchezo mmoja tu," alisema Hamdi
Yanga ilitua Zanzibar mapema jana na jioni kikosi kilipata nafasi ya kukamilisha maandalizi yake ya mwisho katika uwanja wa mazoezi wa Amaan