Wakati Yanga ikisubiri kumtambulisha kocha mpya wa timu hiyo aliyechukua mikoba ya Miloud Hamdi ambaye alijiunga na Ismailia ya Misri, inaelezwa kocha huyo tayari ametoa mapendekezo juu ya kambi ya maandalizi 'pre-season'
Romain Folz raia wa Ufaransa ndiye anatajwa kuwa mkufunzi wa Yanga, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe akidokeza kuwa kocha huyo tayari yuko nchini kwa wiki kadhaa
Kwa mujibu wa taarifa, Folz amependekeza Yanga kuweka kambi ya maandalizi Misri akihitaji kambi itakayokuwa na utulivu na miundo mbinu yote ambayo atahitaji katika maandalizi yake
Mapendekezo hayo huenda yakavuruga mipango ya awali ikiwa ni pamoja na kufuta mpango wa Yanga kushiriki michuano maalum ya pre-season nchini Namibia
Hata hivyo Yanga itaanzia Rwanda ambabo itashiriki mechi maalum katika maadhimisho ya Rayon Sport Day, August 15
"Tumeshabadilisha timu ina kocha tayari na amekuja na mapendekezo yake, kule Namibia na Afrika Kusini hakutaendeka tena kocha amekataa na ametuagiza tutafute sehemu ya kwenda lakini iwe ndani ya Misri," kiongozi wa Yanga alinukuliwa na Mwanaspoti
"Ametupa sababu na tumezielewa na yanafanyiwa kazi haraka nadhani timu ikiondoka hapa kwenda Rwanda kwenye ile mechi ya Rayon haitarudi hapa tena iteelekea huko. Anataka wachezaji wote wa timu yake wawepo kwenye safari hiyo kasoro hawa ambao wako kwenye mashindano ya CHAN ambao nao itategemea na hatua watakayofikia"
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema wiki hii na ijayo watakamilisha zoezi la utambulisho wa kikosi, kocha na benchi lake la ufundi na wiki ijayo wachezaji wanapaswa kurejea kambini kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya mwanzoni wa August 2025