Baada ya mapumziko hapo jana, Yanga inatarajiwa kuendelea kutambulisha nyota wapya waliojiunga na mabingwa hao wa nchi
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema jana walitoa nafasi maalum kuenzi mahusiano yao na Safari Lager ambapo shamrashamra za fainali ya Safari Lager Cup zilifanyika uwanja wa KMC Complex zikihitimishwa na mchezo kati ya Safari Lager talents dhidi ya Yanga uliomalizika kwa Wananchi kuibuka na ushindi wa bao 1-0
Yanga ni mshirika wa Safari Lager katika program ya kusaka vipaji ambapo zoezi hilo lilifanyika nchi nzima kupata kikosi kilichochuana na Yanga jana
Kamwe amesema wataendelea kuwatambulisha wachezaji wao wapya zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kikosi kuanza maandalizi ya msimu
"Zoezi la utambulisho wa wachezaji litaendelea Jumapili (leo) baada kumalizika kwa fainali za Safari Lager Cup ambapo sisi Yanga ni mshirika mkuu wa Tamasha hili"
"Sisi hatufichi wachezaji wetu tuliowasajili kama bangi, pia hatuna sababu ya kufanya mbwembwe nyingi nje ya uwanja"
"Tumefanya usajili mzuri na tunaamini kila mchezaji tuliyemsajili atadhihirisha hilo uwanjani," alisema Kamwe
Mpaka sasa Yanga imetambulisha usajili wa nyota wanne wapya ambao ni Moussa Balla Conte, Abdulnasir Mohammed 'Casemiro', Offen Chikola na Lassine Kouma