Meneja wa klabu ya Yanga, Walter Harrison, ameweka wazi kuwa maandalizi ya kikosi hicho kuelekea msimu mpya wa mashindano ya 2025/26 yanaendelea kwa mafanikio makubwa.
Yanga ipo kambini Avic Town, ikiwa imeingia rasmi siku ya tatu ya mazoezi baada ya kuanza maandalizi yao kwenye dimba la KMC Complex.
Harrison amesisitiza kuwa kipindi cha pre-season ndicho msingi wa mafanikio ya timu, kwani ndicho kinachojenga uimara wa wachezaji kimwili, kiakili na kimbinu kuelekea msimu mrefu wa mashindano.
“Tumekuwa na nyakati nzuri tangu tulipoanza pre-season yetu, leo tukiwa na siku ya tatu hapa Avic Town. Hiki ni kipindi cha maandalizi, na wachezaji wanafahamu sio kipindi chepesi kwao,” alisema Harrison.
Ameeleza kuwa mazoezi yamekuwa na viwango tofauti vya ugumu lakini wachezaji wameonyesha nidhamu na uvumilivu mkubwa kwa kuelewa umuhimu wa maandalizi hayo.
Aidha, Harrison hakusita kutoa pongezi kwa kocha mkuu Romain Folz na benchi lake la ufundi kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha timu inakuwa tayari kwa ushindani.
“Kwa dunia ya leo makocha vijana ndio wenye soko kubwa. Romain ni aina ya kocha ambaye sehemu kubwa ya maisha yake ni mpira wa miguu. Akiamka asubuhi yeye ni mpira tu, na hata pale anapokuwa nje ya majukumu ya uwanjani, yuko kwenye kompyuta akiandaa program za mazoezi au kufanya vikao muhimu vya kimkakati,” alisema.
Harrison alimalizia kwa kuonyesha matumaini makubwa kuwa kufikia mwanzo wa msimu, Yanga itakuwa tayari kutimiza malengo yake na kuendelea kuwa tishio katika medani za soka ndani na nje ya Tanzania.