Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amewahakikishia wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa chini ya kocha Romain Folz watarajie mambo makubwa kutoka kwa timu yao
Kamwe amesema ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Wiliete S.c ambao Yanga wameupata ugenini juzi ni dalili ya uimara wa kikosi cha Folz ambacho kilitoka kucheza mechi ya dabi dhidi ya Simba na kusafiri kwa zaidi ya saa 7
“Yanga imecheza Dabi ya Kariakoo tarehe 16 kuanzia saa 11 jioni, mechi inaisha kufika saa 3 usiku timu inarejea hotelini, hakuna kulala, wachezaji wanachukua nguo zao moja kwa moja saa 7 usiku wanafika uwanja wa ndege kujiandaa na safari ya kwenda Angola"
“Alfajiri saa 10 tarehe 17 wachezaji wanasafiri hadi Ethiopia, pale wanapumzika kwa saa tatu, hakuna aliyefunga jicho.
“Wanatoka pale wanaunganisha ndege kuja Angola takribani saa tatu hadi nne angani, wanafika wanapumzika, hakuna aliyefanya mazoezi. Tumepata siku moja tu ya kufanya mazoezi halafu leo (juzi Ijumaa) tumekwenda kwenye mechi kucheza dhidi ya timu ya pili kwa ubora Angola. Tumeitawala karibia kila eneo"
“Tumetengeneza nafasi, tumemiliki mpia na kuwa bora katika kila eneo. Angalia ratiba ilivyobana halafu unaona Yanga inatawala Angola"
“Kinachopikwa na Romain Folz, Mwenyezi Mungu atupe tu uhai mje mshuhudie bomu linalotengenezwa. Pengine kauli ya rais wetu (Hersi Said) aliyosema msimu huu tuna timu bora kuliko miaka yote minne, kwa mtu anayejua mpira ataanza kuona mabadiliko ya kikosi yanayofanyika"
"Tumecheza ugenini bila ya Dickson Job na hakuna aliyekumbuka kama hayupo, ameingia Bakari Mwamnyeto amecheza na Ibrahim Bacca. Maxi na Mudathir waliocheza Dabi, wamekaa benchi, tumeanza na watu wengine, hakuna aliyezungumza Mudathir yuko wapi wala kwa nini Maxi hakuanza"
“Hapa kati tuna mechi ya ligi (dhidi ya Pamba Jiji itakayochezwa Septemba 24 mwaka hu), halafu hawa Waangola wakija nyumbani ndiyo mechi ambayo Yanga tunakwenda kujaribu kila kitu chetu kwenye Ligi ya Mabingwa"
“Siku hiyo tutakuwa makini sana kwa sababu tunataka kufuzu kwa idadi kubwa ya mabao kwani kuna goli la mama, hapa pekee tumechukua milioni 15, huenda mechi ya marudiano tukaongeza jitihada tukachukua hata milioni 30 za mama, inawezekana"
"Katika hatua hii ya awali tunataka kukusanya mabao mengi zaidi ili tupate hela nyingi kutoka kwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan,” alitamba Kamwe.