Kocha Mkuu wa Yanga Romain Folz jana aliendeleza rekodi yake ya ushindi wa asilimia 100 akiwaongoza Wananchi kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wiliete SC katika mchezo wa mkondo wa pili hatua ya awali ligi ya mabingwa barani Afrika
Ushindi huo umeihakikishia Yanga kutinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 5-0
Folz ameiongoza Yanga katika mechi nne za mashindano na amefanikiwa kushinda zote pasipo kuruhusu bao
Chini yake katika mechi hizo, Yanga imefunga mabao tisa ikishinda 1-0 dhidi ya Simba, 3-0 na 2-0 dhidi ya Wiliete, 3-0 dhidi ya Pamba Jiji
Licha ya changamoto ya ratiba ambapo kwa wastani kikosi chake kimeshuka dimbani kila baada ya siku tatu, Folz amefanikiwa kubeba alama tatu
Silaha yake kubwa ni 'rotation', Folz ameonyesha ujasiri kwa kufanya mabadiliko ya kikosi katika kila mechi, mpaka sasa mfumo huo umemlipa
Bado kuna malalamiko kutoka kwa baadhi ya mashabiki wanaoamini kuwa timu yao haichezi vyema. Lakini kwa kuzingatia muda ambao Folz amekaa na timu pamoja na ratiba ya kucheza kila baada ya siku tatu, sio muda sahihi wa kumhukumu kocha
Mwanzoni mwa msimu uliopita Yanga ilipitia kipindi kigumu cha mechi mfululizo kama hivi wakati huo ikinolewa na kocha Miguel Gamondi, mwenendo ulikuwa wa kusuasua hadi pale ilipopoteza mechi mbili na Gamondi kuonyeshwa mlango wa kutokea
Hata kocha aliyechukua nafasi yake Sead Ramovic alianza na vipigo viwili kwenye ligi ya mbingwa na kama asingepata matokeo katika mechi zilizofuta pengine angeondoka mapema
Folz kwa wakati huu anapata matokeo mazuri, ameshinda mechi zote tangu alipokabidhiwa jukumu la kuinoa Yanga
Kuna kipindi cha mpito ambacho kila kocha mpya anaweza kupitia kabla mifumo na mbinu zake kuingia katika vichwa vya wachezaji
Kwa sasa unaweza kusema Yanga inapita katika kipindi hicho, ni suala la muda tu vile vipigo vya 5G vitarejea