Baada ya taarifa za ujio wa kocha mkuu wa Kaizer Chiefs, Nasreddine Nabi, jijini Dar es Salaam, mitaani na mitandaoni kumeibuka tetesi nyingi zikimhusisha na vilabu vikubwa vya Tanzania, hususan waajiri wake wa zamani Yanga SC, na hata watani wao wa jadi Simba SC, ambao bado wako sokoni wakisaka kocha mpya.
Hata hivyo, taarifa za uhakika zinaeleza kuwa kocha huyo amekuja nchini kwa ajili ya mapumziko akiwa na familia yake. Nabi mwenyewe amesisitiza wazi kuwa hajaja kufanya mazungumzo ya kikazi na timu yoyote, bali anatumia nafasi hiyo kujipumzisha kutokana na presha ya kazi yake Afrika Kusini.
Kwa sasa, Nabi yupo kwenye mgogoro na waajiri wake Kaizer Chiefs baada ya kusimamishwa kupisha uchunguzi juu ya kile kilichodaiwa kuwa udanganyifu katika taarifa za leseni yake ya ukocha.
Kwa upande wa Yanga, kocha Romain Folz yuko kwenye presha kubwa baada ya kiwango kisichoridhisha cha timu yake. Hali hii imechochea sauti za baadhi ya mashabiki kutamani urejeo wa Nabi, ambaye aliondoka Jangwani kwa heshima kubwa akiacha alama ya mafanikio.
Nabi aliipa Yanga mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu ya NBC na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF (CAF CC) mafanikio ambayo bado yanakumbukwa na mashabiki wa Wananchi.
Pamoja na kuondoka Yanga, Nabi ameendelea kudumisha uhusiano mzuri na mdhamini mkuu wa klabu hiyo, GSM. Kila mara anapokuwa nchini, amekuwa akitembelea nyumbani kwa mfadhili huyo, jambo linalowasha zaidi uvumi wa uwezekano wa kurejea kwake siku moja.