Ukifuatilia mijadala mitandaoni tangu Yanga itangaze kuwa mashabiki wataingia bure katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers Jumamosi, utaona sauti tatu tofauti: wanaoshangilia uamuzi huo, wanaoupinga na wale wanaojifanya wachambuzi huru lakini kiukweli wana ajenda zao.
Kinachosisitizwa na wanaoupinga si hoja ya kiufundi. Hawazungumzii hamasa. Hawazungumzii nguvu ya umati. Hawataji uhalisia wa mchezo husika kwamba presha yake inahitaji nguvu ya mashabiki na sio viti vitupu. Wao wanasema ni hasara, ni matumizi ya ovyo lakini hawasemi moja kwa moja jambo walilolificha: hawapendi kuona Yanga inasonga mbele.
Mashabiki wasipoteze muda kwa kejeli
Hawa wanaoponda leo ndiyo hao hao watakaokaa viti vya mbele Jumapili kwenye vipindi vya uchambuzi redioni wakichambua na kufurahia Yanga kushindwa kufuzu makundi ya CAFCL.
Hao hawatoshi kuwa kipimo cha busara ya Yanga, maana hii ni mechi ya Wananchi, na Wananchi wameomba jambo lao: kuingia bure ili kujaza uwanja na kutoa nguvu ya kiroho, kiakili na kiushindani kwa wachezaji wao.
Yanga ni klabu ya Wanachama, wameamua
Yanga si kampuni ya mtu mmoja, ni taasisi ya wanachama. Uongozi haukubuni; umetii kilichoombwa na wamiliki halali wa klabu. Ukisikia maoni hasi ambayo hayatoki kwa wanachama wala mashabiki, elewa hapo kuna hisia za kutamani Yanga isifaulu.
Si mara ya kwanza, ni utamaduni
Hii sio mara ya kwanza Yanga kuingiza mashabiki bure uwanjani. Huu ni utamaduni wa kuheshimu mchango wa mashabiki, umeanza tangu enzi za akina Hayati Yusuf Manji, na huja tu pale panapohitajika nguvu ya pamoja kuliko hesabu ya kiingilio. Na Jumamosi ni moja kati ya hizo siku.
Yanga inahitaji ushindi wa kuanzia 2–0. Mkakati wa kwanza wa ushindi ni kujaza uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mtu anayekwambia “kujazana bure si hoja” hajawahi kuona jinsi goli la tatu linaweza kupatikana dakika ya 89 kwa sababu ya vuvuzela na makelele ya watu 50,000 waliokaa upande wako.
Hii si mechi ya mijadala, ni mechi ya Wanayanga na jambo muhimu kwa Wananchi ni kwenda uwanjani kuipa sapoti timu yao halafu warudi nyumbani vifua mbele baada ya dakika 90