Kocha Msaidizi wa Yanga Patrick Mabedi amesema wako tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC ambao utapigwa kesho Jumapili Novemba 09 katika uwanja wa KMC Complex.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari mapema leo, Mabedi alisema wanatambua umuhimu wa mchezo huo wakizihitaji alama tatu ili kuendele kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi.
"Tunashukuru maandalizi yetu yanakwenda vizuri, tulirejea mazoezini siku ya Jumatano na nisema tu tumejiandaa vyema kukabiliana na KMC ambayo inafundishwa na kocha mzuri"
"Hii ni mechi muhimu sana kwetu kupata alama tatu ili kuendelea kujiweka vyema katika msimamo wa ligi. Tunafahamu haitakuwa rahisi kwa sababu hakuna timu nyepesi kwenye ligi hii"
"Hatutawadharau wapinzani wetu kwa kuangalia nafasi waliyopo katika msimamo wa ligi, tunauchukulia mchezo huu kwa umuhimu mkubwa," alisema Mabedi
Mabedi aliongeza kuwa wamefanyia kazi eneo la ushambuliaji ili kuhakikisha wanatumia vyema nafasi nyingi wanazotengeneza.
"Katika mechi zilizopita tumekuwa na changamoto ya kufunga lakini jambo jema kwetu ni kuwa tunatengeneza nafasi nyingi"
"Hivyo tumefanya kazi kwenye uwanja wa mazoezi ili kuhakikisha tunaongeza ufanisi katika safu yetu ya ushambuliaji"