Mabingwa watetezi ligi kuu ya NBC Yanga leo wako uwanjani dimba la KMC Complex kuikabili KMC katika mwendelezo wa ligi.
Inaweza kuwa nafasi kwa Yanga kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi kwa mara ya kwanza msimu huu endapo Wananchi wataibuka na ushindi katika mchezo huo.
Wanakutana na KMC ambayo bado inajitafuta chini ya kocha kutoka Brazil Marcio Maximo ambaye pia amewahi kuinoa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania.
KMC wanaburuza mkia katika msimamo wa ligi wakikusanya alama tatu kutoka mechi tano ambapo wameshinda mechi moja na kufungwa nne.
Hata hivyo KMC ni timu isiyotabirika inapokutana na Yanga, vijana wa kocha Pedro Goncalves watahitaji kupambana ili kuondoka na alama zote tatu.
Baada ya kukiandaa kikosi chake kwa takribani siku nne, mashabiki wa Yanga leo wanaweza kupata mwanga wa aina ya soka ambalo watalishuhudia chini ya Mreno huyo.
Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kikosi chake kamili, ni mshambuliaji Clement Mzize pekee ambaye atakosekana akiwa ni majeruhi huku beki Ibrahim Bacca akiendelea kutumikia adhabu ya mechi tano alizofungiwa.
Mchezo unatarajiwa kupigwa saa 10 jioni.