Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi CAFCL dhidi ya AS FAR ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari mapema leo, Goncalves alisema licha ya kutambua ugumu wa kundi B linalotajwa kama kundi la kifo, alisema hiyo ni fursa kwao kushindana dhidi ya timu bora na kudhihirisha ubora wao.
Amesema AS FAR wamejipambanua kwa kuwa na timu nzuri lakini hata Yanga pia ina kikosi bora chenye wachezaji wenye vipaji vikubwa.
"Kesho ni mchezo wetu wa kwanza kwenye hatua ya makundi, kila mtu anasema ni kundi la kifo kwa sababu ya timu kubwa nne. Lakini kama unataka kuwa bingwa lazima ushindane na mabingwa."
"FAR Rabat wana timu nzuri ambayo ina wachezaji bora. Sisi tuna timu bora sana ambayo ina muunganiko mzuri pia. Tukipata hamasa ya kutosha kutoka kwa mashabiki basi tutakuwa na mchezo bora zaidi," alisema Goncalves
Akizungumzia ubora wa AS FAR hasa eneo lao la kiungo, Goncalves amesema ameiandaa timu yake kimbinu akiamini katika mipango yake.
“Nafahamu wapinzani wetu wamejipanga sana eneo la kiungo. Nina wachezaji 32, isipokuwa nina wachezaji wawili ambao wapo majeraha. Mmoja wao ni Clement Mzize ambaye ningependa kuchukua nafasi hii kumpongeza sana kwa kushinda tuzo ya goli bora afrika nina imani tuzo hii itampa hamasa ya kupambana ili kurejea uwanjani na ari kubwa”
“Falsafa yangu ni kuutawala mchezo kwa gharama yoyote ile. Nahitaji wachezaji wangu wajitume sana. Malengo yangu makubwa ni timu kucheza vizuri. Matokeo ya mchezo wa kesho naamini yatatokana na namna ambavyo tutacheza vizuri."
"Mimi naamini matokeo mazuri yanatokana na namna ambavyo tutaongeza utulivu na umakini. Dhamira ya wana Yanga wanahitaji siku moja kushinda taji la Afrika. Bado tupo kwenye mchakato bora wa kufika tunapohitaji kufika."
"Haijalishi ni lini tutapata hilo kombe lakini dhamira ndio kitu muhimu. Kama tukiendelea na mradi huu basi tutafikia malengo. Kama tunahitaji kusonga mbele tunapaswa kujifanyia tathmini ya namna gani tinachukua hatua kwenye mchezo,” alisema Goncalves