Mikiki mikiki ya ligi ya mabingwa hatua ya makundi inaingia raundi ya pili ambapo leo mechi nne zitapigwa.
Mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga wao watakuwa ugenini huko Algeria kuikabili JS Kabylie katika mchezo wa kundi B.
Baada ya kuanza vyema hatua ya makundi kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS FAR, wababe hao wa soka Tanzania leo wana nafasi nyingine ya kuwania alama tatu ili kuendelea kujiweka kwenye nafasi nzuri katika mkakati wa kuisaka tiketi ya robo fainali.
Hata hivyo mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 1 usiku unatarajiwa kuwa mgumu, JS Kabylie wametoka kupoteza mchezo uliopita kwa kufungwa mabao 4-1 dhidi ya Al Ahly hivyo mchezo wa leo ni kama fainali kwao.
Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari jana, Mkufunzi wa Yanga Pedro Goncalves alisema hana wasiwasi wowote kuelekea mchezo huo kwani wamejiandaa kukabiliana na presha ya wenyeji wao ambao wanatarajia kujaza uwanja unaochukua mashabiki 50,700.
Goncalves alisema vijana wake wana uzoefu wa kucheza katika mazingira hayo hivyo anaamini watakwenda kutimiza vyema mpango wao wa mchezo huo na muhimu zaidi ni kutafuta ushindi.
Yanga iliweka kambi ya maandalizi yake hapo Algeria kwa takribani siku tatu, huku wakipata siku mbili za kujifua nchini humo.