Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga jioni ya leo watashuka dimba la KMC Complex kuikaribisha Fountain Gate katika mwendelezo wa ligi kuu ya NBC.
Baada ya dakika 180 za kibabe katika michuano ya ligi ya mabingwa, leo Wananchi wanarejea kwenye msako wa taji la tano mfululizo ligi kuu ya NBC.
Ni Djigui Diarra Day! Ndivyo Wananchi wanavyosema mechi hii ikitumika 'kumheshimisha' Diarra ambaye amekuwa na mchango wa aina yake kwenye kikosi cha Yanga tangu alipojiunga na Wananchi misimu minne iliyopita.
Itakuwa mechi ya tatu ya ligi kwa kocha Pedro Goncalves aliyeanza vyema majukumu yake katika kikosi cha Yanga akiwaongoza Wananchi kushinda mechi tatu katika mashindano yote na sare moja.
Hii ni moja kati ya mechi mbili za viporo ambazo Yanga itacheza wiki hiii kabla ya ligi kusimama kwa takribani wiki sita kupisha michuano ya Afcon 2025
Baada ya mchezo dhidi ya Fountain Gate, Wananchi wataelekea mkoani Dodoma kuikabili Coastal Union katika mchezo mwingine utakaopigwa Jumapili