Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate hapo jana, kikosi cha Yanga hakina muda wa kupoteza kwani wanaelekea mkoani Dodoma kwa ajili ya mchezo mwingine wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union.
Jumapili Disemba 07 Yanga itashuka uwanja wa Jamhuri kuwakabili wenyeji wao Coastal Union ambao wamechagua kutumia uwanja wa Jamhuri baada ya uwanja wao wa Mkwakwani kufungwa na Bodi ya Ligi ukikosa sifa.
Ushindi dhidi ya Fountain Gate jana umeisogeza Yanga hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 13 kutoka mechi 5 walizocheza mpaka sasa.
Wananchi wanaweza kusogea hadi nafasi ya pili kama watapata ushindi dhidi ya Coastal Union na pengine kusalia katika nafasi hiyo hadi pale ligi itakaporejea tena baada ya michuano ya Afcon 2025 itakayofanyika mwishoni mwa mwezi huu huko Morocco.