Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amesema hawako tayari kusikiliza kauli za kuwakatisha tamaa kwani wanajiamini, Jumapili watapata ushindi dhidi ys JS Kabylie na kukata tiketi ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika (CAFCL).
Kamwe ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kikosi kurejea kutoka Morocco ambako walipoteza mchezo wa raundi ya tano kwa bao 1-0 dhidi ya AS FAR.
Kamwe ametamba kuwa Yanga ina uzoefu na mechi za maamuzi hivyo Jumapili watakwenda kuwafunga midomo wote wenye mashaka na uwezo wa mabingwa hao wa soka Tanzania Bara.
"Hatuhitaji mtuamini kwa sababu sisi Yanga wenyewe tunajiamini na tunajua tutakachoenda kukifanya siku ya Jumapili. Nyie pigeni hesabu zenu halafu malizeni maneno."
"Mimi nasema Yanga itakuwa timu pekee kutoka Tanzania itakayocheza robo fainali ya mashindano ya CAF msimu huu."
"Nazungumza kwa kujiamini kabisa, sina mashaka Jumapili Yanga inakwenda kufuzu robo fainali. Kama kuna hesabu pigeni nyinyi mjimalize."
"Saa tutaenda kumshona mtu pale New Amaan Complex na saa tatu tutaanza sherehe ya kwenda robo fainali," alitamba Kamwe
Yanga inahitaji ushindi wa angalau mabao 2-0 dhidi ya JS Kabylie huku ikiomba Al Ahly wapate ushindi dhidi ya AS FAR ili kusonga mbele hatua ya robo fainali.
Kinachowapa moyo Wananchi ni kuwa Al Ahly hawajapata ushindi katika mechi tatu mfululizo zilizopita kwenye mashindano yote hivyo mechi dhidi ya AS FAR wanaichukulia kwa umuhimu mkubwa kwani matokeo tofauti yanaweza kushuhudia kocha wa timu hiyo akifutwa kazi.
Lakini jukumu la kwanza la Yanga ni kushinda mechi dhidi ya JS Kabylie kabla ya kufikiria matokeo ya Al Ahly kwani kama Yanga itakosa ushindi, AS FAR watatinga robo fainali pasipo kujali matokeo yao dhidi ya Al Ahly.