Klabu ya Yanga inakabiliwa na wakati mgumu kutokana na mfululizo wa majeraha yanayowakumba wachezaji wake.
Wakati mabingwa hao watetezi ligi kuu ya NBC wakijiandaa kuikabili TRA United katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid siku ya Jumatano, uongozi wa Yanga umethibitisha kukosekana kwa mastaa wanne ambao wamebaki jijini Dar es salaam wakiwa majeruhi.
Taarifa iliyotolewa na Yanga jana imebainisha kuwa beki wa kati Ibrahim Bacca alipata jeraha la nyonga kwenye mchezo uliopita dhidi ya Azam Fc hivyo atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki tatu.

Mshambuliaji Laurindo Aurelio 'Depu' naye amepata changamoto ya nyama za paja pia akitarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki mbili.
Pia wamo Chadrack Boka anayesumbuliwa na enka na Edmund John ambaye bado anasumbuliwa na bega wote wakitarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili.
Nyota hao wanaungana na beki Dickson Job na kiungo mshambuliaji Clement Mzize ambao wao watakuwa nje ya uwanja hadi mwishoni mwa msimu baada ya kufanyiwa upasuaji Afrika Kusini hivi karibuni.