Wakati uongozi wa Young Africans SC (Yanga) ukimuweka kikaangoni kocha mkuu Pedro Goncalves, kuna dalili kwamba baadhi ya wachezaji waliokuwa hawapati nafasi wanaweza kunufaika na mabadiliko yanayoweza kufanyika ndani ya kikosi hicho.
Taarifa zinaeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo unahitaji maelezo ya kina ya kiufundi kutoka kwa Goncalves, hasa kuhusu sababu za kutowatumia baadhi ya wachezaji katika kipindi chote cha duru ya kwanza ya msimu.
Miongoni mwa wachezaji walioathirika zaidi na hali hiyo ni kiungo Salum Abubakar maarufu kama Sure Boy na Farid Mussa ambao hawajaonekana kabisa katika mipango ya kikosi tangu ujio wa kocha huyo huku Kibwana Shomari yeye akiwa na nafasi finyu.
Ajabu ni kwamba, hata katika kipindi ambacho Yanga ilikuwa ikikabiliwa na wimbi la majeruhi ya wachezaji kadhaa muhimu, majina ya wachezaji hao hayakujumuishwa kwenye kikosi cha mechi mbalimbali.
Kibwana ametumika zaidi kwenye mechi za kombe la CRDB wakati Farid na Sure Boy wakikosa kabisa nafasi kwenye mashindano yote.
Katika misimu iliyopita, Sure Boy alikuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Yanga, akicheza nafasi muhimu ya kiungo wa kati kwa ufanisi mkubwa. Hali hiyo pia ilionekana kwa Farid Mussa ambaye ni mchezaji kiraka ambaye alitumika katika maeneo tofauti.
Kutotumika kwao ghafla msimu huu kumeibua maswali mengi kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka, wakitaka kufahamu sababu za kiufundi zilizopelekea hali hiyo.
Inaelezwa kuwa uongozi wa Yanga unatafuta majibu iwapo maamuzi hayo yalitokana na mbinu za kocha, kiwango cha wachezaji au sababu nyinginezo za ndani ya timu.
Iwapo maelezo hayo hayatakuwa na mashiko, kuna uwezekano wa kufanyika kwa mabadiliko yatakayowapa nafasi wachezaji hao na pengine kuanza kuonekana tena kikosini.