Yanga umeagiza benchi la ufundi kuhakikisha wachezaji wote waliopo kikosini wanapata nafasi ya kucheza, kufuatia tathmini ya kina ya mwenendo wa timu iliyofanyika mwanzoni mwa wiki.
Katika kikao hicho, makocha waliwasilisha ripoti yao kwa viongozi wakieleza mafanikio na changamoto walizokutana nazo, hasa katika mwezi wa Machi ambao ulikuwa na msongamano mkubwa wa michezo ya mashindano mbalimbali.
Ripoti hiyo pia ilihusisha tathmini ya mchango wa kila mchezaji mmoja mmoja ndani ya kikosi, jambo lililowezesha viongozi kubaini kuwa baadhi ya wachezaji hawajapata nafasi ya kutosha huku wengine wakionekana kuwa na mchango mdogo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamw amesema viongozi walihoji sababu za hali hiyo na kutaka maelezo ya kina kutoka kwa benchi la ufundi.
Alisema kocha aliwasilisha majibu ya kiufundi kuhusu upangaji wa kikosi, lakini maelezo hayo hayakuwekwa wazi hadharani.
Hata hivyo, Kamwe alibainisha kuwa viongozi wameweka msimamo thabiti kuwa kila mchezaji anapaswa kupewa nafasi ya kucheza, akisisitiza kuwa wote wanalipwa kwa ajili ya kuitumikia timu.
“Viongozi wameelekeza wazi kuwa kila mchezaji anahitajika kupewa nafasi, hasa katika kipindi hiki ambacho timu ina michezo mingi ya mashindano mbalimbali,” alisema.
Aliongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha kikosi kizima kinakuwa tayari wakati wote na kuongeza ushindani wa ndani, huku pia ikisaidia kupunguza uchovu kwa wachezaji wanaotumika mara kwa mara.
Hatua hiyo ni habari njema kwa baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa na nafsi finyu kwenye kikosi kwani sasa wanaweza kuanza kuonekana kwenye baadhi ya mechi kwa kuzingatia mahitaji ya kiufundi.
Kilio cha mashabiki wa Yanga ambao walitamani kuwaona tena wachezaji kama Farid Mussa na Salum Abubakar 'Sure Boy' huenda sasa kikawa kimesikika.