Klabu ya Simba SC hivi karibuni ilifungua malalamiko rasmi kupinga uhalali wa uraia wa kiungo wa Yanga, Mohamed Damaro Camara, akidaiwa kusajiliwa kama mchezaji wa ndani bila kufuata taratibu stahiki.
Shauri hilo limesikilizwa leo na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kwa ajili ya uchunguzi zaidi, huku Simba ikiliwakilishwa na Mwanasheria wake Adv. Hosea Chamba
Kamati imesikiliza hoja za klabu ya Simba bila ya uwepo wa Damaro wala klabu ya Yanga.
Yanga kutohudhuria kwa shauri hilo lililoitwa kwa mara ya pili na Kamati ni kusisitiza msimamo ambao Wananchi wameuweka kuwa usajili wa Damaro waliukamilisha kwa kufuata taratibu zilizowekwa na mamlaka ya soka nchini (TFF).
Yanga ilimsajili Damaro mwezi Januari kwenye usajili wa dirisha dogo akiwa tayari ni raia wa Tanzania. TFF ikathibitisha uhamisho wake kujiunga na Yanga kama Mtanzania.
Pengine Simba hawakupaswa kuishitaki Yanga wala Damaro kwenye shauri hilo. Damaro hakujileta Yanga, amejiunga baada ya usajili wake kuidhinishwa na TFF.Β
Simba walipaswa kupeleka hoja zao TFF au uhamiaji kama wana mashaka na U-Tanzania wa Damaro.
Kwa sababu Yanga haiwezi kuwapa majibu kuhusu U-Tanzania wa Damaro kwani ipo mamlaka ya Uhamiaji inayohusika na masuala hayo.
Lakini pia ni TFF iliyomuidhinisha Damaro kujiunga na Yanga kama Mtanzania, sasa kama Simba wana mashaka na hilo walipaswa kwenda kuwauliza TFF.
Hoja zinazoibua maswali mengi ni kuhusu hatua hii ya kuishitaki Yanga na mchezaji Damaro wakati jambo la msingi linazihusu mamlaka zaidi.