Mikiki mikiki ya ligi kuu ya NBC inaendelea leo ambao mabingwa watetezi Yanga wako jijini Mwanza wakikabiliwa na mchezo dhidi ya Pamba Jiji.
Ni mechi muhimu kwa Wananchi kuzisaka alama zote tatu ili kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi. Hata hivyo, wanakutana na timu iliyojipambanua na rekodi ya aina yake nyumbani.
Msimu huu Pamba Jiji hawajapoteza mchezo wowote uwanja wa CCM Kirumba wakifanikiwa kupata sare dhidi ya vigogo wengine wa jiji la Dar es salaam Simba na Azam Fc.
Kwa Yanga alama tatu zitakuwa na maana kubwa kwao katika mpango wa kutetea ubingwa kwa msimu wa tano mfululizo.
Baada ya watani zao Simba kudondosha alama katika mchezo dhidi ya Azam Fc, ni motisha kwa mabingwa hao watetezi kusaka ushindi dhidi ya Pamba Jiji ili kunufaika na matokeo hayo ya watani zao.
Yanga ilitua Mwanza juzi usiku na jana kikosi kikapata nafasi ya kufanya mazoezi ya mwisho katika dimba la CCM Kirumba.
Mkufunzi wa Yanga Pedro Goncalves amekiri vijana wake watahitaji kuwa katika ubora ili kushinda mchezo huo.
Goncalves alisisitiza kuwa Yanga haiko kileleni mwa msimamo wa ligi kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na uimara wa kikosi chao hivyo wanakwenda katika mchezo huo kuzisaka alama zote tatu.