Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo raundi ya 19 ambapo mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga watakuwa dimba la KMC Complex kuikaribisha Mbeya City.
Ni mechi nyingine muhimu kwa Wananchi kuzisaka alama tatu ili kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kabla ya kuelekea visiwani Zanzibar kushiriki kombe la Muungano.
Hautakuwa mchezo mwepesi kwa Wananchi kwani Mbeya City ni moja ya timu tano zilizoweza kuchukua alama kwa vinara hao wa ligi msimu huu.
Mechi ya kwanza iliyowakutanisha mkoani Mbeya ilimalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana.
Ni matokeo hayo ambayo yalipelekea Yanga kufanya maboresho ya benchi la ufundi wakimfuta kazi Romain Folz nafasi yake ikichukuliwa na Pedro Goncalves ambaye tangu ajiunge na Wananchi hajapoteza mchezo kwenye ligi.
Yanga inaelekea kwenye mchezo huo ikiwa na ahueni ya majeruhi nyota wengi waliokuwa nje wakiwa tayari kurejea kikosini.
Ni wachezaji wawili tu Emmanuel Mwanengo na Buba Jammeh ambao wanaendelea na matibabu huku mshambuliaji Depu akiendelea na mazoezi ya fitness baada ya kupona majeraha.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa saa 12:30 jioni..