Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema wamejiandaa kikamilifu kwa mchezo wa nusu fainali kombe la Muungano dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa New Amaan Complex.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo katika mkutano na wanahabari visiwani Zanzibar, Goncalves alisema anatarajia mchezo huo utakuwa mgumu kwa kuwa timu mbili bora zitakutana.
Pedro amesema licha ya muda mfupi wa maandalizi, watakuwa tayari kuwakabili Azam Fc wakiwa na lengo la kufuzu hatua ya fainali.
"Tunatarajia kuwa na mchezo wa ushindani mkubwa, Azam FC ina wachezaji bora, kila tunapokutana nao wanatupa ushindani mkubwa. Hivyo tunatarajia itakuwa nusu fainali yenye ushindani mkali kutoka kwa kila timu."
"Lakini licha ya uboa wao, sisi tumejiandaa vyema kuhakikisha tunatoa ushindani wa hali ya juu na kutimiza malengo yetu kwenye mchezo huu muhimu."
"Tumefanya maandalizi yetu kwa umakini mkubwa, ingawa tuna changamoto ya ratiba ngumu ya michuano hii sambamba na mechi nyingine za ligi zinazoendelea,"alisema Goncalves
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo, watakamilisha maandalizi ya mwisho leo tayari kwa mtanange huo ambao utaamua timu itakayotangulia fainali kabla ya mchezo wa pili wa nusu fainali kati ya Mlandege dhidi ya Simba utakaopigwa Jumapili