Tangu arejee kutoka kwenye majeruhi, mshambuliaji wa Yanga Prince Dube amekuwa katika kiwango bora.
Dube jana aliiongoza Yanga 'kuikanda' Azam Fc mabao 2-1 katika mchezo wa nusu fainali kombe la Muungano na mabingwa hao watetezi kutinga fainali.
Mshambuliaji huyo wa Kimatifa wa Zimbabwe alihusika katika mabao yote mawili akifunga bao la kwanza baada ya pasi adhimu kutoka kwa Allan Okello 'Star Boy' na baadae kutengeneza bao la pili lililofungwa na Maxi Nzengeli pia Dube akipokea pasi kutoka kwa Okello.
Dube sasa amepachika mabao matano katika mechi tatu zilizopita. Ndiye kinara wa mabao katika michuano ya kombe la Muungano akiwa na mabao matatu aliyofunga kwenye mechi mbili.
Ushirikiano wake na Okello umeanza kuwa tatizo kubwa kwa walinzi wa timu pinzani kwani mabao mawili kati ya matatu aliyofunga Zanzibar yamepita kwnye mguu wa Okello.