Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema wanauchukulia kwa umuhimu mkubwa mchezo wa fainali kombe la Muungano dhidi ya Simba utakaopigwa leo Jumatano, April 29 katika uwanja wa New Amaan Complex.
Kamwe amesema thamani kubwa ya mchezo huo inatokana na ukweli kuwa ni fainali ambapo mshindi ataondoka na taji la ubingwa.
Amesema kutokana na mazingira hayo, Yanga inakwenda kucheza soka la kushambuliaji na hawatajali kama mchezo huo utamalizika kwa idadi kubwa ya mabao kufungwa.
"Huu ni mchezo wa fainali ni tofauti na mchezo wa ligi ambao hata alama moja kwetu ni matokeo mazuri. Hivyo wafahamu kabisa tunakwenda kushambulia mwanzo mwisho"
"Hatutajali kama tutafungana mabao 10 au zaidi jambo muhimu ni kuwa Yanga inayokwenda kucheza fainali leo ni tofauti kabisa na ile iliyocheza March 1"
"Sisi mwamuzi akipuliza kipyenga cha kuanzisha mchezo tu, tutakuwa golini kwao," alitamba Kamwe.
Yanga ndio mabingwa watetezi na leo watakuwa wakisaka taji la pili tangu michuano hiyo iliporejeshwa miaka miwili iliyopita.