Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo ambapo mchezo mmoja wa kuhitimisha raundi ya 20 utapigwa. Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga watakuwa ugenini dimba la Meja Jenerali Isamuhyo kuwakabili wapinzani wao wa jadi klabu ya Simba.
Ni mchezo mwingine mkubwa unaozikutanisha timu hizo zenye upinzani wa kihistoria. Ni takribani siku tano zimepita tangu timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa fainali kombe la Muungano visiwani Zanzibar Yanga ikikubali kipigo cha bao 1-0 na kupoteza taji hilo kwa watani zao.
Leo ni mchezo wenye sura tofauti kwa sababu matokeo yake yanaweza kutoa mapema mwelekeo wa mbio za ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
Endapo Yanga itaibuka na ushindi, kimahesabu itakuwa imejiweka katika nafasi nzuri ya kutetea taji lao, kwani watakuwa juu ya msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama nane.
Maana yake ni kuwa katika mechi 10 zitakazokuwa zimesalia, Wananchi watahitaji kushinda angalau mechi 7 na pengine sare moja tu kutetea taji lao.
Sare bado itaiweka Yanga kwenye nafasi nzuri kwani watalinda gap la alama tano lililopo sasa.
Lakini mambo yanaweza kuwa tofauti endapo Yang itapoteza mchezo huo, bado itakuwa kileleni lakini kwa tofauti ya alama 2. Hayo ni matokeo ambayo Wananchi hawahitaji kwani yanaweza kuwaongezea presha kuelekea mechi zilizobaki kuhitimisha msimu.
Yanga inatarajiwa kushuka dimba la Isamuhyo ikiwa na dhamira moja tu, USHINDI ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kurejesha ubingwa Jangwani kwa msimu wa tano mfuulizo.
Wananchi pia wanahitaji kulipa kisasi baada ya kipigo walichokutana nacho kutoka kwa watani zao Jumatano iliyopita. Ikumbukwe kabla ya kupoteza mchezo huo, Yanga ilikuwa imecheza mechi 7 mfululizo bila kupoteza dhidi ya Simba.
Hivyo ni matokeo ambao hayakuwafurahisha Wanayanga na leo watakuwa na nafasi ya kuendeleza ubabe wao dhidi ya Simba ili kuendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo kwenye ligi kwa zaidi ya mechi 40.
Yanga ilikamilisha maandalizi yake uwanja wa Isamuhyo jana licha ya hali ya uwanja kutoridhisha kutokana na mvua iliyonyesha jijini Dar es salaam jana.
Ni wazi itakuwa mechi ngumu lakini kutokana na umuhimu wake, matokeo ya USHINDI ni kipaumbele cha kwanza kwa Yanga.