Nani kakwambia mechi ya mpira wa miguu unashinda kwa dakika 10? Nani alikwambia ushindi unapatikana kwa mwanzo mzuri pekee? Kama kuna jambo dabi ya jana imetufundisha, basi ni kwamba mpira hauamuliwi na mwanzo bali na uimara wa dakika zote 90.
Katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, tulishuhudia simulizi halisi ya msemo huu. Ndani ya dakika 10 za mwanzo, Yanga walikuwa tayari nyuma kwa mabao 2-0. Kwa macho ya wengi, huo ungeweza kuwa mwanzo wa anguko. Lakini kwa wachezaji wa Yanga, ulikuwa mwanzo wa mapambano.
Kilichofuata ni hadithi ya ari, nidhamu, na moyo wa kutokata tamaa. Taratibu wakarejea mchezoni, wakadhibiti presha, na hatimaye wakasawazisha hadi kufikia sare ya 2-2 dhidi ya watani wao wa jadi. Huu haukuwa tu mchezo wa soka, bali ulikuwa somo la kisaikolojia kwamba mchezo hauishi hadi filimbi ya mwisho.
Dabi hii haikukosa changamoto zake nje ya uwanja. Masuala ya mazingira ya mchezo yaliendelea kuwa sehemu ya mjadala, ikiwemo uamuzi wa Yanga kutotumia vyumba vya kubadilishia nguo na badala yake kupanga sehemu nyingine karibu na uwanja baada ya kubaini hali isiyo ya kawaida nyumbani. Hii inaonyesha namna ambavyo dabi hizi zinavyobeba presha si tu kwa wachezaji bali hata kwa mifumo ya maandalizi.
Kwa upande wa Simba, zile dakika 10 za mwanzo zilileta matumaini makubwa kwa mashabiki wao. Lakini matumaini hayo yalififia kadri muda ulivyoenda na Yanga kuanza kuonyesha makali yao. Baada ya hapo, mashabiki walibaki wakitazama mchezo kwa wasiwasi mkubwa, wakiona kasi na mbinu za wapinzani wao zikiongezeka.
Kipindi cha pili kilikuwa na ushindani mkubwa zaidi. Yanga walionekana kuwa na nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi kwa kuzingatia nafasi walizopata kama wangezitumia vyema.
Lakini pia kama ilivyo kawaida, mijadala ya maamuzi ya waamuzi haikukosekana. Licha ya waamuzi wote kutoka nje ya nchi (Morocco) yapo makosa mengi walifanya. Tukio la beki Ismail Toure kumpiga kiwiko mshambulizi Depu ndani ya eneo la hatari lilizua maswali mengi, likiwa mojawapo ya matukio ambayo yangelibadilisha mwelekeo wa mchezo.
Zaidi ya hapo, makosa ya waamuzi wasaidizi kwenye maamuzi ya kuotea yalionekana wazi, yakikatiza mashambulizi hatari ya Yanga mara kadhaa. Wakati mwingine tunawaadhibu waamuzi wetu kutokana na tu na presha kutoka nje lakini kiuhalisia waamuzi wa mchezo wa jana hawana tofauti na waamuzi wengi wanaochezesha hapa nchini.
Licha ya yote, matokeo ya sare yanaacha ladha tofauti kwa kila upande. Kwa Yanga, ni matokeo yenye thamani kubwa, wanabaki kileleni mwa msimamo wa ligi wakiwa na tofauti ya alama tano. Kwa Simba, ni sare ambayo inafifisha matumaini yao kwenye mbio za ubingwa.