Yanga imerejea juu ya msimamo wa ligi kibabe baada ya kuibamiza Singida BS mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa KMC Complex.
Shoo za Allan Okello 'Star Boy' zimeendelea kushuhudiwa pale KMC Complex leo akiweka kambani mabao mawili sasa akimfikia mshambuliaji Prince Dube ambaye kabla ya mchezo huo alikuwa akiongoza wafungaji wa mabao ndani ya Yanga akiwa nayo 9.
Okello aliweka kambani bao la kwanza dakika 14 kwa mpira wa adhabu ambao ulimuacha mlinda lango Metacha Mnata asijue la kufanya.
Baada ya kufungwa bao hilo, benchi la ufundi la Singida BS lilifanya mabadiliko ya mlinda lango Metacha akimpisha Amos Abasogie.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakuisaidia Singida BS kwani waliruhusu bao la pili kabla ya mapumziko kwenye dakika ya 42 likiwekwa kambani na Mudathir Yahya alimalizia shambulizi ambalo awali liliokolewa na mlinda lango.
Pengine Yanga ilipaswa kwenda mapumziko na ushindi mnono zaidi kama Maxi Nzengeli, Okello na Mudathir wangetumia vyema nafasi walizopata.
Kipindi cha pili ni Yanga iliyoendelea kutawala na kutengeneza nafasi nyingi lakini bado ufanisi ulikosekana kwenye umaliziaji.
Hata hivyo alikuwa ni Okello aliyefunga bao la tatu kwenye dakika ya 69 likiwa bao lake la 9 msimu huu.
Ni ushindi unaoifanya Yanga ifikishe alama 57 na kurejea rasmi kileleni mwa msimamo wakiwaacha watani zao Simba kwenye nafasi ya pili wakiwa na alama 55.




