Yanga ilitua mkoani Kigoma jana na kupata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki wao mkoani humo kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mashujaa Fc ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Lake Tanganyika.
Mapokezi hayo yalikuwa na maana kubwa kwa wachezaji wa Yanga na benchi la ufundi ambapo wameahidi hawatawaangusha kwenye mchezo huo.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake kuelekea mchezo huo, mlinda lango Hussein Masalanga amesema wamepata heshima ya kipekee mkoani humo na sasa ni zamu yao kuwapa mashabiki wao furaha pale dimba la Lake Tanganyika.
"Tangu tulipowasili tumepokea mapokezi mazuri sana kutoka kwa mashabiki wetu wa Kigoma. Walikuja kwa wingi kutupokea na hata walihudhuria mazoezi yetu ya jana."
"Tunafurahi sana kuwaona na tunataka kuwapa burudani nzuri kesho kama njia ya kuthamini upendo na sapoti yao. Wachezaji wote tupo tayari na mchezo wa kesho na malengo yetu ni kufanya vizuri kwenye michezo yote iliyosalia," alisema Masalanga.
Yanga leo inatarajiwa kufanya mazoezi yake ya mwisho kwenye uwanja wa Lake Tanganyika tayari kwa mchezo huo utakaopigwa saa 10 Alasiri.
Vinara hao wa ligi kuu ya NBC wanahitaji ushindi ili kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi na kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.