Baada ya ushindi muhimu wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa Fc jana, kikosi cha Yanga kinarejea Dar leo kabla ya kuelekea mkoani Arusha wanakokabiliwa na mchezo mwingine dhidi ya Fountain Gate utakaopigwa Jumatano, Juni 17 uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema watakuwa na siku moja ya mapumziko kabla ya kuelekea mkoani Arusha.
Kamwe amesema wanauchukulia mchezo dhidi ya Fountain Gate kwa tahadhari kubwa wakihitaji kushinda ili kuendelea kuukaribia ubingwa wa tano mfululizo.
"Fountain Gate ni timu ngumu, niliwaona walivyocheza dhidi ya Azam Fc licha ya kuwa walipoteza. Tunakwenda Arusha tukiwa na tahadhari kubwa tukifahamu aina ya timu tunayoenda kukutana nayo," alisema Kamwe.
Katika mechi nne zilizobaki, Yanga inahitaji kuvuna angalau alama 10 ili kujihakikishia ubingwa mwingine kwa msimu wa tano mfululizo.