Kesho Jumatano Yanga itashuka uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar kuikabili Azam Fc katika mchezo muhimu wa ligi kuu ya NBC.
Mchezo huo wa raundi ya 28 umebeba matumaini ya Wananchi kwenye mbio za ubingwa msimu huu.
Ni siku mbili tu zimepita tangu timu hizo zilipokutana jijini Mwanza kwenye mchezo wa nusu fainali kombe la CRDB Yanga ikikubali kipigo cha mabao 3-2 katika mchezo uliopigwa kwa dakika 120.
Matokeo hayo yameongeza presha kwenye mchezo wa kesho huku Wananchi wakifahamu kama watapoteza mchezo huo basi wataweka rehani matumaini yao ya kutetea ubingwa wa ligi kuu kwa msimu wa tano mfululizo.
Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikihitaji matokeo ya aina moja tu, USHINDI ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa.
Pamoja na kuwa zimesalia mechi tatu msimu kufika tamati, mchezo dhidi ya Azam Fc unatizamwa kama mchezo unaoweza kuamua hatma ya ubingwa kwa Yanga.
Ushindi kwa Yanga utapunguza presha kuelekea mechi mbili zitazobaki dhidi ya TRA United na JKT Tanzania lakini matokeo tofauti hasa kupoteza yanaweza kuongeza presha kwenye mechi hizo zilizobaki kwani inaonekana wazi watani zao Simba wanaweza kushinda mechi zote zilizobaki.
Habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kuwa nyota wa timu hiyo wanakwenda kuikabili Azam Fc wakiwa na morali ya juu hasa kutokana na matokeo ya mchezo uliopita.
Hakuna mchezaji ambaye yuko tayari kuona wanapoteza mechi nyingine dhidi ya Azam Fc katika kipindi cha siku tatu.
Baada ya nusu fainali ya kombe la CRDB, hii sasa itakuwa kama fainali...